Social Icons

Tuesday, 12 August 2014

JIFUNZE ZAIDI: UFAHAMU WA MIUJIZA YA MUNGU NA MIUJIZA YA MANABII WA UONGO


Askofu mkuu Zachary Kakobe.

UFAHAMU KUHUSU MIUJIZA YA MUNGU NA JINSI YA KUZIFAHAMU ISHARA NA AJABU ZA UONGO ZA SHETANI NA MANABII WAKE WA UONGO
NENO LA MSINGI:

2 WATHESALONIKE 2:9:

“Yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa KUTENDA KWAKE SHETANI, KWA UWEZO WOTE, NA ISHARA NA AJABU ZA UONGO.”

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>

Katika somo la leo la Kanisa la Nyumbani, tunajifunza somo muhimu linaloambatana na majira tuliyo nayo ya nyakati za mwisho. Siku hizi, mahali pengi duniani ikiwamo Tanzania, kumezuka watu wa kila namna wakisema ni watumishi wa Mungu na kwamba wamepewa karama ya kutenda miujiza kwa ajili ya kuwasaidia watu. Kwa sababu hii, watu kila mahali wanamiminika kuwafuata, wakihitaji watoto au uponyaji mbalimbali wa mwili. Sehemu nyingine watu hao wanaodaiwa kuwa ni watumishi wa Mungu, wanatumia maji ya baraka kuponya; wengine wanatumia sanamu ya Bikira Maria; wengine wanawapeleka watu makaburini; wengine wanakwenda kupewa maji mahali inaposemekana alitokea Bikira Maria; wengine wanapewa madaftari ambamo humo wameandikiwa kwamba “Mungu” amesema watazaa mtoto wa kiume na wameandikiwa jina la kumwita, au mtoto wa kike na jina ambalo “Mungu” amemchagulia, na kupeleka madaftari hayo kila mara kuombewa na kukatazwa kwenda kliniki n.k. Wengine wamebeba “mimba” zilizotokana na maombezi ya watu hawa kwa miaka miwili bila kujifungua na kupata mateso makali mno. Wengine wameshuhudia kwamba wamepona kabisa baada ya kuhudumiwa na watu wa jinsi hiyo. Hapa ndipo penye mtego. Ili tusinaswe na mitego ya namna hii, Kanisa la Mungu linapaswa kufahamu Biblia inasema nini kuhusu Miujiza, Ishara na Ajabu za Mungu na zile za Shetani.



SHETANI ANA UWEZO WA KUFANYA MIUJIZA, ISHARA NA AJABU ZA UONGO

Miujiza kadhaa kwa kipimo kidogo cha uwezo ulio na mpaka. Wakati wana wa Israeli walipokuwa hawajatoka Misri, waganga na wachawi wa Farao, walifanya miujiza kwa uwezo wa shetani:

(a) Wachawi hawa walipozibwaga fimbo zao chini, ziligeuka kuwa nyoka kwa mfano wa muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni [SOMA KUTOKA 7:8-12]



(b) Wachawi hawa walifanya muujiza wa kubadilisha maji kuwa damu kwa mfano wa muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni [SOMA KUTOKA 7:19-22].



Unaona! Shetani ana uwezo wa kufanya miujiza na ishara. Biblia inasema katika:

UFUNUO WA YOHANA 16:14:

“Hizo ndizo roho za MASHETANI, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote, kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.”

Wakati wa dhiki Kuu, roho za Mashetani zitafanya ishara kubwa, hata kufanya moto kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. [SOMA UFUNUO 13:11-13].

Lakini pamoja na ufahamu huu ulio nao sasa kwamba Shetani ana uwezo wa kufanya ishara na miujiza, bado inakupasa kufahamu jambo moja. Shetani ana mpaka katika uwezo wake wa kufanya miujiza. Hana uwezo wa Mungu wa KUTENDA MAMBO YOTE. Shetani hawezi kutenda mambo yote. Wachawi na waganga wa Farao ingawa walifanya miujiza tuliyoiona, hata hivyo walishindwa kufanya muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni; pale walipoyabadilisha mavumbi ya nchi kuwa chawa. Wachawi hao waliposhindwa walikiri mbele ya Farao kwamba uwezo wa Mungu uko juu mno kuliko uwezo wao. [SOMA KUTOKA 8:16-19]. Wachawi na waganga wa Farao pia walishindwa kuzuia majipu yenye kufura yaliyotumbuka juu ya wanadamu wote wa Misri kutokana na mavumbi aliyoyarusha Musa hewani. Wachawi hao nao walipigwa majipu hayo [SOMA KUTOKA 9:8-11]. Fimbo ya Haruni ilizimeza fimbo za wachawi kudhihirisha uwezo wa Mungu ulivyo mkubwa mno kuliko wa majeshi yote ya shetani [SOMA KUTOKA 7:11-12].

ISHARA, AJABU NA MIUJIZA YA SHETANI WAKATI WOTE INA LENGO LA KUWAPOTEZA WANADAMU ILI WAANGAMIZWE

MATHAYO 24:24:

“Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu WAPATE KUWAPOTEZA, kama yamkini, hata walio wateule.”

Ishara, ajabu na Miujiza ya Shetani ndiyo maana inaitwa pia “NGUVU YA UPOTEVU” kwa jinsi ambavyo miujiza hiyo ilivyo madanganyo ya udhalimu kwa hao wanaopotea ambao hawataki kuiamini kweli ya Mungu na kuokolewa na hatimaye kuzidi kuipenda kweli katika wokovu. Nguvu hiyo ya upotevu juu ya wanadamu, hatimaye inawafanya wanadamu hao kuhukumiwa na kwenda Jehanum ya moto. [SOMA 2 WATHESALONIKE 2:7-12]. Kwa sababu hii, Kanisa la Mungu lazima liwe macho na kufahamu waziwazi jinsi ya kuzifahamu ishara, ajabu na miujiza ya Shetani na kutofautisha na ile itokanayo na Mungu. Kwa maarifa haya, ni rahisi kuziepuka kazi zote za Shetani na manabii wake; na pia kuwasaidia wengine waliokwisha kunaswa.

ALAMA TISA ZINAZOAMBATANA NA ISHARA, AJABU NA MIUJIZA

INAYOTOKANA NA MUNGU

Kwa kuangalia alama hizi tisa zifuatazo, na kuhakikisha kwamba ZOTE ZINAKUWEPO; ndipo tunapoweza kuzitambua ishara, ajabu na miujiza inayotokana na Mungu na kuifahamu na kukwepa miujiza ya Shetani na manabii wake:

(1) Mtu anayetumiwa kufanya ishara, ajabu au miujiza na Mungu, inabidi awe ameamini au kuokolewa; akikiri mwenyewe wokovu ulio katika Kristo Yesu na kuushuhudia.

MARKO 16:17; “Na ishara hizi zitafuatana na hao WAAMINIO …..”.

Mtu yeyote asiyeokolewa na kukiri wokovu na kuushuhudia, hawezi kufanya miujiza itokanayo na Mungu. Miujiza hiyo hutokana na Shetani.

(2) Huduma ya Uponyaji au Ishara yoyote inayotokana na Mungu lazima iambatane na Biblia au Neno la Mungu kwa kuwa Neno la Mungu ndiyo dawa ya Ugonjwa na tena ndilo linalofanya

miujiza. Huduma yoyote ya uponyaji wa miujiza isiyoambatana na Biblia au Neno la Mungu, inatokana na Shetani.

ZABURI 107:20: “HULITUMIA NENO LAKE, HUWAPONYA, huwatoa katika maangamizo yao.”

MITHALI 4:20-22: “Mwanangu, SIKILIZA MANENO YANGU; ….UZISIKIE KAULI ZANGU …..MAANA NI UHAI kwa wale wazipatao, na AFYA YA MWILI WAO WOTE.”

YOHANA 6:63: “…..MANENO HAYO NILIYOWAAMBIA niroho tena NI UZIMA.”

(3) Huduma yoyote ya Uponyaji wa Miujiza inayotokana na Mungu, LAZIMA iambatane na kuhubiri Injili na kufundisha Neno la Mungu, Angalia maandiko:

(a) HUDUMA YA YESU:

(i) Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, KULIAMBATANA na kuwahubiri maskini habari njema [SOMA LUKA 4:18].

(ii) Yesu alipokuwa akifundisha Neno la Mungu ndipo uweza wa Bwana ulipokuwapo kuponya:

LUKA 4:17:


“Ikawa siku zile mojawapo ALIKUWA AKIFUNDISHA …. NA UWEZA WA BWANA ULIKUWAPO APATE KUPONYA.”

(4) YESU ALIPOWATUMA WANAFUNZI KUFANYA HUDUMA YA UPONYAJI

Wakati wote Yesu Kristo alipowatuma wanafunzi wake na kuwapa uwezo wa kuponya maradhi, au kuwaambia wapoze wagonjwa kwa miujiza; jambo hilo LILIAMBATANA na kutumwa kuhubiri au kuutangaza ufalme wa Mungu. Mambo haya mawili lazima yaende pamoja.

LUKA 9:1-2: “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma WAUTANGAZE UFALME WA MUNGU NA KUPOZAWAGONJWA.”

LUKA 10:1-2, 9: “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine,sabini, akawatuma wawili wawili …. Akawaambia … WAPOZENI WAGONJWA waliomo, WAAMBIENI, UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA.”

MATHAYO 10:7-8: “Na katika kuenenda kwenu, HUBIRINI,mkisema, Ufalme wa Mbinguni umekaribia. POZENI WAGONJWA, FUFUENI WAFU, TAKASENI WENYE UKOMA, TOENI PEPO; mmepata bure, toeni bure.”

Katika kujifunza juu ya Huduma ya Yesu ya miujiza na uponyaji, na ile ambayo aliwapa wanafunzi wake; umeona kwamba kuponya wagonjwa kwa miujiza na kufanya ishara na ajabu zinazotokana na Mungu, LAZIMA kuambatane na kuhubiri Injili, na kuwaambia watu watubu dhambi zao na kuokolewa maana ufalme wa Mungu umekaribia. Ukimwona mtu anasema ni mtumishi wa Mungu na kwamba eti amepewa karama na Mungu kuponya wagonjwa, halafu akawa nyumbani kwake tu au ofisini kwake na watu wanamwijia kuponywa bila kuelezwa habari za kutubu na kuokolewa, ufahamu huyo ni nabii wa uongo, na anatumia NGUVU YA UPOTEVU ya Shetani kufanya ishara za uongo. Uponyaji wa Miujiza wa Mungu hauwi kama hospitali ambapo watu wanaenda kupewa vidonge tu bila kuhubiriwa Injili. Miujiza lazima iambatane na kuhubiri Injili. Mtu ukimsikia anasema yeye amepewa karama na Mungu kuponya wagonjwa tu, lakini hakupewa karama ya kuhubiri; hivyo kuhubiri amewaachia wengine, ujue huyo ni nabii wa uongo. Yeyote aliyepewa kufanya miujiza na Mungu, pia huyohuyo atahubiri Injili. Yesu, Petro, Paulo, Filipo na yeyote katika Biblia walifanya miujiza PAMOJA NA kuhubiri Injili.

Uponyaji wowote, muujiza wowote, au ishara yoyote inayofanywa kutokana na Mungu LAZIMA IFANYWE KWA JINA LA YESU SOMA: LUKA 10:17; MATENDO 4:30; MARKO 16:17; MATENDO 3:6; MATENDO 4:10; MATENDO 3:13, 16; MATENDO 16:18. Jina la Yesu, ndilo linalomtia mtu dhaifu, nguvu. Imani katika Yesu ndiyo inayoleta uzima [MATENDO 3:16]. Ukimwona mtu anayejiita mtumishi wa Mungu na kwamba anaombea wagonjwa, lakini halitumii Jina la Yesu ila anamtaja “Mungu” tu; ujue mtu huyo ni nabii wa uongo. Hakuna muujiza wowote wa Mungu pasipo kulitaja jina la Yesu! “PEPO WANATUTII KWA JINA LAKO”, “KWA JINA LANGU WATATOA PEPO.” Siyo kwa jina la Mungu au kwa kumtaja Mungu ila kwa jina la Yesu. LAZIMA Yesu atajwe katika kuufanya muujiza unaotokana na Mungu.

(5) Mtu anayetumiwa kufanya miujiza, ishara au ajabu na Mungu, hukusanya pamoja na Yesu, na kutumia miujiza kuliongeza Kanisa la Mungu kwa wale waaminio au wanaookolewa. Lengo la Mungu kutoa uwezo wa kufanya miujiza kwa watumishi wake, ni kuwafanya wasioamini waweze kuamini kwa kuziona nguvu za Mungu. Huduma yoyote ya miujiza isiyokuwa na lengo la kuwaongeza walioamini kwa Bwana Yesu au katika Kanisa la Mungu siyo huduma ya Mungu.

MATENDO 5:12,14:

“Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; ….walioamini wakazidi kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake”.

Miujiza hutumika kukusanya watu na kuwaleta katika Kanisa ambalo kiongozi wake ni Yesu[SOMA PIA LUKA 11:23; MATHAYO 23:37; ZABURI 50:5].

No comments:

Post a Comment