THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Kiongozi wa
Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu
Mkuu Moses Kulola ambaye ameaga dunia , Alhamisi, Agosti 29, 2013
katika Hospitali ya AMI iliyoko Masaki mjini Dar Es Salaam akiwa na umri
wa miaka 84.
Rais
kikwete ameelezea mshtuko na huzuni yake katika Salamu za Rambirambi
alizomtumia Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Bwana Brown Mwakipesile kufuatia
kifo cha Askofu Mkuu Kulola.
“Nimeshtushwa,
nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa
Mungu wa muda mrefu na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies
of God Tanzania (EAGT), Marehemu Moses Kulola kutokana na maradhi
yaliyomfanya wakati fulani apelekwe hadi India kupatiwa matibabu” amesema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Askofu Moses Kulola kwa miaka mingi
wakati wa enzi za uhai wake, kama Mtumishi Hodari wa Kiroho aliyejitoa
vilivyo katika kuwahudumia Waumini wa Kanisa lake ambapo mahubiri yake
yametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani za Waumini wake na
kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi
yetu.
Aidha
Rais Kikwete amesema kifo cha Askofu Mkuu, Moses Kulola kimeacha pengo
kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa lake hapa nchini, bali pia miongoni
mwa wapenda amani kote nchini na kwingineko duniani kwa vile enzi za
uhai wake, Marehemu aliweza kufikisha ujumbe muhimu wa kiimani kupitia
mahubiri yake kwa watu wa mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la
Afrika.
“Kwa
niaba yangu mwenyewe na Serikali ninayoingoza, ninakutumia wewe Katibu
Mkuu wa Kanisa la Evangelical Assembies of God Tanzania, Bwana Brown
Mwakipesile na Waumini wote wa Kanisa hilo Salamu za Rambirambi kutoka
dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Kiongozi muhimu wa Kiroho.
Ninawajulisha kuwa niko nanyi katika wakati huu mgumu kwa sababu msiba
wenu ni msiba wetu pia. Sala na mioyo yetu iko nanyi wakati wa
maombolezo ya kifo cha Kiongozi huyo shupavu wa dini. Nawaomba wote muwe
wavumilivu na wenye subira kwani yote ni Mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.
“Vilevile
kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole
nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu, Askofu Mkuu, Moses
Kulola kwa kumpoteza Baba, Kiongozi Shupavu na Mhimili wa familia.
Natambua fika kwamba hiki ni kipindi kigumu sana kwao cha maombolezo.
Natambua machungu yenu wakati huu na naungana nanyi katika kumwomba
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke peponi roho ya Marehemu Moses
Kulowa. Amina.”
Mazishi ya Marehemu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) yatafanyika
mjini Mwanza Jumatano ijayo tarehe 4 Septemba, 2013. Heshima za mwisho
kwa mwili wa Kiongozi huyo zitatolewa siku ya Jumamosi tarehe 31
Agosti, 2013 katika Kanisa laEAGT karibu na Hospitali ya Temeke kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013
No comments:
Post a Comment