Social Icons

Saturday, 24 May 2014

Bila Neema ya Mungu hatufai mbele zake!

neema1

2KORTHO 12:7-17 na RUMI 8:26-27

Kila mtu hata aliyeokoka ana udhaifu rundo, na hasa udhaifu wa kuzitegemea akili zetu badala ya kumtegemea Mungu katika maisha yetu; tunao upungufu wa kifedha kwa ajili ya mahitaji yetu mbalimbali; huo nao ni udhaifu; udhaifu wa afya na wengine ulemavu kabisa wa viungo baadhi; udhaifu katika kuomba mbele za Mungu, udhaifu katika kufikiri; udhaifu wa kihisia n.k

“UDHAIFU: Siyo dhambi au uovu ndani yetu kama wengi wanavyodhani, bali ni ule upungufu au uhitaji wa mambo ya kimwili na kiroho tulio nao ambao hatuna uwezo nao sisi wenyewe bila Mungu tu aingilie kati.

Note: Haisaidii kukana kuwa huna udhaifu au kujitetea au kujaribu kuficha , tukubali mbele za Mungu kuwa sisi ni dhaifu ili Roho Mtakatifu atusaidie udhaifu wetu.

- Pale mtu anapojiona dhaifu, Mungu atamtumia sana kuliko anayejiona kuwa ana nguvu maana mtu dhaifu muda wote wa maisha yake atamtegemea Mungu tu. Hii ndiyo maana ya Mtume Paulo hasa pale anaposema kuwa anajisifia udhaifu wake kwa furaha nyingi ili uweza wa KRISTO ukae juu yake. 2Kor 12:9-10

- Paulo AKIJIONA dhaifu na asiyeweza jambo lolote ndipo alipoziona nguvu za Mungu zikichukua udhaifu wake na kumvusha.

2. Ni muhimu kuelewa dhahiri kuwa, sisi kama vyombo vya udongo tunaweza kuvunjika tu saa yoyote kama hatutapata msaada toka kwa Roho Mtakatifu. Rum. 9:19-26: 2Kor 4:7 -10.

 Mbele za Mungu tujapo lazima tukubali kuwa tuna mapungufu badala ya kujifanya kuwa tuna kila kitu, tuwe wakweli na
tuorodheshe udhaifu wetu mbele zake ili atusaidie. Ni Yesu peke yake asiye na udhaifu au uhitaji wa aina yeyote tangu alipofufuka mauti na kuketi mkono wa kuume wa Mungu Baba.

 Lazima tukubali ukweli huu “ sisi sote ni BINADAMU tu” ambao bado tutafikwa na matatizo endapo Mungu ataruhusu yatufike,
haijalishi ni Askofu au Nabii, Mwombaji au Mwinjilisti, ndiyo sababu maisha yetu yote lazima tujifunze kumtegemea Yesu ili
atuvushe.

- Paulo anaridhika na udhaifu aliokuwa nao kwa sababu udhaifu huo ulimfanya amtegemee Mungu katika huduma aliyompa badala ya kutegemea UZOEFU wake; na kwa kweli ukigundua kuwa wewe una udhaifu, na UNAMTEGEMEA mtu mwingine akusaidie udhaifu wako HUTAJIVUNA’. “SISI SOTE NI DHAIFU, TUSIKATAE UKWELI HUU KAMA TUNATAKA KUZIONA NGUVU ZA MUNGU JUU YETU”

3. Mfano
(a) Mwanzo 32:24-30. Sote tunajua maisha ya Yakobo yalivyotegemea ujanja na nguvu za kukimbia na pale alipokutana na Mungu uso kwa uso na kumwomba ambariki, Mungu akamtegua ( aligusa mshipa) (msuli wa paja ndio wenye nguvu kuliko misuli yote mwilini) na tangia siku hiyo Yakobo akatembea kwa kuchechemea, hatumii nguvu zake tena kupambana na Esau ndugu yake; sasa anamtegemea Mungu tu; Badala ya kupambana naye kimwili; sasa anainama. Mwanz. 33:1-20 Haleluya.

(b) Ili tusiwe na kiburi Bwana ametupa zawadi ya udhaifu, kwa lengo la kutufanya kila wakati tujue mipaka yetu: udhaifu wetu daima utatuzuia tusiende mbele kasi mno sisi wenyewe na badala yake tumtangulize Mungu atuwezeshaye. Waamuzi 7:1- 8 (Habari za Gideoni)

- Gidioni kwa udhaifu wake katika kufikiri, alikusanya jeshi la watu 32,000 ili kwenda kupigana na Wamidiani, Mungu akalipunguza hadi kubaki watu 300 tu !! Lengo la Mungu ni kuchukua udhaifu wa Gideoni wa kutegemea jeshi kubwa ndipo ashinde vita, bali amtegemee Mungu akiwa na watu 300 tu ili kushinda jeshi la Midiani lenye askari 135,000

- Baada ya kushinda vita, Israel walijua kuwa siyo nguvu yao iliyo shinda bali Mungu. Waam 8:22-23.

“ ndiyo sababu Mungu huchagua vyombo dhaifu vinavyo mtegemea yeye ili kuviaibisha vyenye nguvu Goliathi aliyejaa majivuno na mavazi ya kutisha akauawa na kijana mdogo tu tena asiye na mavazi ya kutisha ila anamtegemea Mungu, Kijana Daudi. 1Samw. 17: 4 – 10, 31 – 54 na 1Kor.1: 26 – 29. 3

4. UDHAIFU TULIONAO NDIO UNAOCHOCHEA USHIRIKA WETU.
Watu wengi wanaodhani kuwa wanazo nguvu za kutosha hawaoni haja ya ushirika, hawahitaji msaada hata wa mtu yeyote, wanadhani wanajitosheleza, na kwa watu wa jinsi hii hata kumtegemea Mungu ni upuuzi; lakini ebu waaangalie mwisho wao!! Lakini sisi kama tutasokota pamoja nyuzi dhaifu za maisha yetu, itatokea kamba yenye nguvu. Kwa kweli Mungu pekee ndiye Bingwa anayeweza kugeuza udhaifu wetu kuwa NGUVU za ajabu.

Note:
Kama watoto wa Mungu, kujiweka wazi mbele za Mungu kuwa wewe ni dhaifu na kwamba unahitaji msaada wake, huleta AHUENI ya moyo, na hii ndiyo hatua ya kwanza na muhimu sana katika kupata UHURU KAMILI TOKA KWA KRISTO YESU.

Udhaifu wa miili yetu ni mojawapo ya kweli ambazo YESU KRISTO hakupenda kuwaficha wanafunzi wake wa karibu saaana. Math. 26: 41 – Usipoomba tu, mwili unatawala roho.

Sasa:
Badala ya kujitumainia tu sisi wenyewe kama watu tusioweza kushindwa kitu, leo tuione Neema ya Mungu tu inayotusaidia; tumwambie Mungu akamate nguvu zetu tunazojivunia kama alivyofanya kwa Yakobo ili tuweze kumtegemea yeye kwa asilimia 100% katika safari yetu; maana kamwe Mungu hatatutumia na kutubariki kweli kweli kama hatujawa tayari kuchechemea (kutotegemea nguvu zetu na ujuzi wetu na ujanja wetu.)

- Lazima nikubali kuwa mimi ni dhaifu katika ndoa yangu na namhitaji Mungu kuiendesha na kuiboresha.
- Mimi ni dhaifu katika utoaji, na mhitaji Mungu anifundishe utoaji unaompendeza yeye.
- Mimi ni dhaifu katika maombi, lazima namhitaji Mungu anifundishe jinsi ya kuomba.
- Mimi ni dhaifu katika kupenda wengine, Mungu nifundishe kupenda. Mimi ni dhaifu, ni udongo unajitetea sana saa ya majaribu, Mungu nifundishe jinsi ya kustahimili majaribu…

Katika jina la Yesu. Ameni

–REV. L. M. MWIZARUBI

No comments:

Post a Comment