Social Icons

Thursday, 10 July 2014

SOMO: MABADILIKO HUTOKA NJE YA MFUMO (CHANGE IS OUT OF THE SYSTEM).

Huu ndo ufunuo aliokuwa akinipa Yesu siku nzima ya jana na alfajiri ya leo amenipa mzigo nikumegee.

Ebu twende darasani kidogo:

1. Yesu na wanafunzi wake kwenye mashua;
Wakati Yesu "amelala" kwenye mashua, wanafunzi wake "walikuwa macho" wakitazama "upepo unavyokwenda" lakini Yesu "hakuwa hapo" alikuwa "nje ya mfumo" alikuwa amelala.

Wakati "mfumo" unaanza kuzama haikumsumbua Yesu... Taharuki, kelele, vilio na majuto ya wanafunzi "kwenye mfumo" uliokuwa unazama havikuweza "kumnyima Yesu usingizi" au kumfanya akurupuke usingizini.

Walipojaribu kila wanachoweza, na kutumia mbinu zote "zinazosaidia kuokoa mfumo usizame" bila mafanikio ndipo walipoamua kuomba msaada "nje ya mfumo" kwa mtu ambaye yanayoendelea kwenye mfumo "hayaathiri" usingizi, amani na ratiba zake!
Mwalimu Dickson Kabigumila

Na Yesu alipoamka tu, kitu cha kwanza kukigusia kilikuwa ni "mfumo wao" naye alisema, " Kwanini mmeona shaka enyi wa imani haba (wa mfumo dhaifu)? Nitachukuliana na ninyi mpaka lini (Mtaendeleaje kuishi kwenye mfumo dhaifu mpaka lini-Mfumo wa mashaka, kutoamini, kutumia akili na mbinu za kibinadamu badala ya Kanuni za Ufalme wa Mungu)?"

Halafu, baada ya kuonesha mapungufu na tofauti ya mifumo waliyoko ndipo Yesu "Akaurekebisha mfumo wao" kwa kuukemea Upepo uliokuwa unawatesa!

Aliyerekebisha mfumo ni mtu aliyekuwa nje ya mfumo.
Watakaorekebisha mambo ya ndoa, uchumi, familia na malezi, afya, huduma za kijamii, siasa nakadhalika ni watu walioko nje ya mfumo.

Watu wenye kanuni zitokazo juu, zisizozama na mashua inayowazamisha wanafunzi (walioko ndani ya Mfumo).

Siasa haitabadilishwa na wanasiasa wanaotumia mbinu zilezile za rushwa, hongo, sera hewa, nguvu za giza kupata nafasi na uongo. Siasa itabadilishwa na watu wenye mtazamo na mfumo tofauti na wa washenzi walioko kwenye mashua ya siasa inayozama.

Kubadili chama kilichoko madarakani haitabadili mfumo mbovu uliokwishaingia kwenye hivyo vyama pia. Litabadilika jina la chama ila ujinga na upumbavu utaendelea.

Mtu anayebadili wanawake kama nguo, ameshindwa hata maisha yake binafsi, atawezaje kubadili yako?
Mtu aliyeoa mke wa ndoa wa mtu, na kuacha wanawake wengine walioko atawezaje kufanya maamuzi ya maana kwa wengine? Walioko kwenye mfumo hawawezi kuugeuza mfumo!!

2. Kufufuka kwa Lazaro wa Bethania
Ukisoma Yohana 11 utaona habari hii.
Waliokuwa kwenye mfumo walileta taarifa wakisema, "Fanya haraka huku Lazaro amezidiwa na muda wowote atakufa"... Lakini, Yesu "aliyekuwa nje ya mfumo" alikuwa na jibu na mtazamo tofauti!!



Wakati wao wanaona kifo, Aliye nje ya mfumo (Yesu) aliona, "Ugonjwa huo si wa mauti"
Wakati wanaleta taarifa mbaya kwamba, "Yule umpendaye amekufa na tayari ananuka ni siku ya nne" Yesu (aliyeko nje ya mfumo) alikuwa na "ripoti tofauti"... Kwake Yeye, "Lazaro hakuwa amekufa siku nne na hakuwa akinuka" bali "Alikuwa amelala tu na ilihitajika kwenda tu kumuamsha toka usingizini"

Waliokuwa kwenye mfumo ulioshindwa "walikuwa wakilia" ila Yesu aliyeishi nje ya mfumo alikuwa "Analia kwa kuwahurumia wao na mfumo wao mbovu"
Walioko kwenye mfumo walikuwa wamepoteza matumaini na imani yote. Walikuwa wamekata tamaa, hawakuona uwezekano.

Ukiwa kwenye mfumo huwezi kuwa na majibu ya kutatua changamoto zilizoko ndani ya mfumo.
Macho, akili na nguvu yako inakuwa imevurugwa na kinachoendelea kwenye mfumo.

Hawa watu walielewa "hawana majibu" hivyo wakatuma taarifa kwa "aliyeko nje ya mfumo" aje kuwakwamua na kuwasaidia.

Hauwezi kutatua matatizo yaliyoko kwenye mfumo ukiwa ndani ya kanuni na taratibu za mfumo.
Wenye mfumo sahihi na bora nje ya mfumo ulioko ndio wanaoweza kubadilisha mambo yaliyoko.

3. Ukombozi wa Israeli toka utumwani Misri
Wana wa Israeli walikuwa kwenye "mfumo kandamizi wa kitumwa" mara tu baada ya kifo cha mtu ambaye "alikuwa nje ya mfumo- Yusufu"

Yusufu alikuwa Misri kama wao lakini yeye alikuwa "Waziri mkuu" akiutawala "Mfumo wa Misri kwa kanuni za Ufalme wa Mungu"

Waisraeli walikuja Misri wakiufuata "Mfumo wa utawala wa Yusufu na Mungu wa Yusufu" lakini wao binafsi hawakuwa wakiuelewa na kuuishi "Mfumo wa Yusufu wa kutawala ugenini"

Siri ya Yusufu ulikuwa baraka za Isaka na Rebeka waliobarikiwa wakiambiwa, "Wazao wako watamilki malango ya adui zao"

Na Yusufu alianza kuuishi huu Mfumo tangu nyumbani kwa Potifa, Akauishi gerezani mbele ya wafungwa wazawa, Na hatimaye akauishi Ikulu.
Alipokufa tu, na mfumo wake ukafa naye. Kwa mantiki kwamba Waisraeli badala ya kujifunza mfumo wa Yusufu na Mungu wake, walijibweteka tu na mwisho wa siku Yusufu akafa na mfumo wake, wakaishia kuingia kwenye "Mfumo kandamizi wa kitumwa"

Na hili kuwatoa Waisraeli huko, Mungu alijua wazi kwamba wanahitajika/ Anahitajika mtu nje ya mfumo kuwanasua.

Ndio maana Mungu alimtoa Musa nje ya mfumo tangu akiwa kichanga.
Na kupitia mtu "Nje ya mfumo" ndipo Ukombozi ulipatikana.

Hata kwa Joshua, Musa alianza kubadili kuwaza na kufikiri kwake, akaanza kupanda Mfumo mpya ndani yake wa "Kulitafakari Neno mchana na usiku" ili mwisho wa siku aanze "Kuyatafakari yaliyo juu na si yaliyo katika nchi" na ndio maana Musa alipokufa ilikuwa rahisi kwa "Mtu nje ya mfumo wa wana wa Israeli- Joshua" kuchukua kijiti cha Musa na kuwafikisha nchi ya ahadi.

Waliokuwa ndani ya mfumo akina Kora na Hakani walipojaribu kuongoza ndani ya mfumo walifia humo wao na watoto wao.

Haiwezekani kuleta mabadiliko ukiwa ndani ya mfumo.

KWA KANISA:
Mimi na wewe tuliookoka kama tusipohama toka kwenye "Mfumo wa dunia hii" unaowakwamisha wengine na kutumia "Hekima itokayo juu (Yesu na Neno lake)" hakika tutakuwa na maisha mabovu kama waliyonayo wasio na Yesu.
Wakiwa na shida itatukuta na sisi kama wao,
Kinachowaliza kitatuliza sisi pia kama wao,
Kinachoua na kuharibu ndoa zao kitaharibu ndoa zetu pia,
Kinachoua na kuharibu afya zao kitaharibu afya zetu pia,
Kinachoua na kuharibu uchumi wao kitaharibu na kuua uchumi wetu pia,
Dawa pekee ya kututoa nje ya Mfumo unaoitesa dunia ni:

a)Kutoifuatisha Namna ga dunia hii bali kugeuzwa na kuenenda kwenye Mapenzi (kanuni) ya Mungu (Warumi 12:1-2).

b) Kuweka bidii kuyajua maandiko na uwezo wa Mungu/ Nguvu za Mungu (Mathayo 22:29).

c) Kuwekeza muda na pesa kupata maarifa na ufahamu (Mithali 24:3-5).

d) Kufanya bidii kumjua sana Mungu kibinafsi (Ayubu 22:21, Danieli 11:32b).

e) Ushirika na utii kwa Roho mtakatifu (Warumi 8:11,14, Yohana 14:26, Yohana 16:8,13-15).

Tusipotoka nje ya mfumo wa dunia hii, hatutaweza kuigeuza dunia yetu na hatutaweza kuishi maisha ya juu na ya ushindi.

No comments:

Post a Comment