skip to main |
skip to sidebar
Wivu ungekuwa ni ugonjwa…
SOMO: WIVU UNGEKUWA NI UGONJWA,
MADAKTARI WENGI BINGWA WANGEANDALIWA MAANA WATU WENGI SANA WANAUMWA
UGONJWA HUU. MAANDIKO: YOH: 11:45-53
1. UTANGULIZI
Mojawapo ya tatizo ambalo limeleta madhara katika jamii nyingi duniani,
ni wivu; wivu ungekuwa na sura, ungemshangaa hata uliye jirani naye
anayekuchekea kwa nje; Wivu ni ile hali ya kutofurahia mafanikio ya
wengine, ni ile hali ya kukosa furaha na amani moyoni unapojilinganisha
na wengi waliofanikiwa; ni ile hali ya kuwa na maumivu moyoni kwa nini
Fulani ndiye kafanya hivi badala ya mimi; kwa nini Fulani ndiye
aolewe/aowe Fulani badala ya mimi; ni ugonjwa unaokula furaha na amani
ya watu wengi kimya kimya, umesababisha madhara mengi sana kwa watu
wengi, na kwa sababu ni ugonjwa usiopimwa maabara watu wakajulikana kuwa
wanaumwa ili watibiwe, umeendelea kuwa ugonjwa wenye kuleta madhara
makubwa na hasa kwa wana wa Mungu tangu nyakati za Kaini. Mwaz. 4 : 1
-13
- Pamoja na sababu nyingine nyingi walizokuwa nazo Mafarisayo,
Masadukayo pamoja na wakuu wa dini ya Kiyahudi wakati wa Yesu na mitume
wake; sababu mojawapo kubwa ya kumsulubisha msalabani ni wivu; walijua
anakuja kuchukua nafasi zao, watu watawaacha, heshima zao zitaisha na
hivyo kwa kutaka kulinda heshima zao; wakaona bora kumwondoa anayetishia
heshima zao kuondoka!! Wakamtenda, kama mhalifu na mnyanganyi mtu
ambaye hakuwa na hatia.
2. Wivu limekuwa ni tatizo lililojificha sana hata kati ya ndugu na
ndugu!! Mwanzo 30:1 ( Rahel ) anamwonea wivu dada yake kwa nini anazaa
na mimi sizai!! Mwz 3 : 37 :4 ndugu zake Yusufu wanaona wivu/ wanachukia
kwa nini Yusufu anapendwa sana na Baba yetu kuliko sisi!! Mwz: 37:20,
Mdo 7:9
- Unafanya vyema kuliko bossi wako na kupata heshima kwa watu bossi
wako hakuambii, lakini ndani yake kama wivu ungekuwa na sura ungeiona.
1Samwel 18 : 5 – 9.
- Sauli alijaribu kujikaza kwa kumchukua Daudi nyumbani kwake na
kumfanya kuwa mchukua silaha zake waendapo vitani lakini ndani ugonjwa
wa wivu unamla – anapanga namna ya kumwondoa tu!! 1 Samwel 18 : 10 – 29;
INATISHA MTU AKIWA NA UGONJWA HUU WA WIVU!! Hana furaha hadi amwondoe
mtu mwenye haki!!
- Watawala wengi sana duniani wameaagamiza watu wengi sana hodari kwa
hofu ya kuchukua nafasi zao; na hata katikati ya wateule Mitume
walipambana sana na roho ya wivu maana ingewamaliza!! Yak. 4:1 – 2, Yak.
3: 14
- Hii roho iliyowatesa sana Wayahudi enzi ya injili ya Mitume. Mdo
13: 42-52, 17:1-9!! Yaani wivu ni roho ya ajabu sana inamtafutia tu mtu
sababu ili kumharibia sifa yake ili kumwangamiza pasipo sababu ya
msingi!! Hii inanikumbusha kisa Fulani cha Askofu Mkuu wa dini Fulani
aliyemwonea wivu makamo wake eti kwa nini mikutano yake ya injili watu
wanakusanyika wengi kuliko mikutano yake!! akaamua kumsimamisha
asihubiri mwaka mzima??
3. Kwa wakati huu nataka niwaambie wote walio na ugonjwa huu wa wivu
kwamba kadri utakavyozidi kuwa na wivu kwa mafanikio ya wengine, ndivyo
daima utakavyozidi kushushwa na Mungu chini zaidi na yule unayemwonea
wivu na kupanga njama za kumwua atazidi kustawi zaidi. 2Smweli 3:1. Hii
ndiyo kanuni ya Mungu.
- Kadri walivyomtesa Yesu na kumzomea na kumwaibisha ili watu wamwite
mlaaniwa, ndivyo Yesu alivyopata umaarufu zaidi duniani baada ya
kufufuka, na hakuna Mfalme yeyote leo hii duniani anayefikia umaarufu
alio nao Yesu Kristo katika jamii.
- Kadri ndugu zake Yusufu walivyomwonea wivu na kumtesa na kumuuza,
ndivyo kadri alivyopata umaarufu machoni pa Farao kuliko wataalamu wake
wote aliokuwa nao na baadaye kuinuliwa zaidi na zaidi. Mwanzo 41 : 37 –
45; Haleluya.
4. Dawa ya wivu ni kuacha kujilinganisha na wengine, acha kuwahukumu
wengine maana mojawapo ya dalili za wivu ndani ya mtu ni pale
anapojikuta hafurahii mafanikio ya watu wengine zaidi ya kuona makosa
yao!! Ni pale anapoanza kujiona kuwa wao wana neema na upendeleo kuliko
yeye; nasema kweli kama vile mchwa wanavyokula nguo taratibu taratibu,
ndivyo wivu unavyokula kiroho cha mtu na baraka zake. Mchwa ukishakula
nguo za mtu anatengeneza tope Fulani juu yake; na wivu nao ukishamwingia
mtu unakula na kutupilia mbali kabisa mafanikio yake. Wivu ndiyo njia
ya mkato na fupi sana anayotumia ibilisi kuharibu mafanikio ya mtu hata
kama ni kihuduma. Na hakuna jambo linalomrudisha mtu aliyeokoka nyuma
kwa haraka sana kama kujaribu kujilinganisha na watu wengine katika
viwango ambavyo wamevifikia kwa muda mrefu!!
- Kaini alimwonea wivu ndugu yake, akaishia kulaaniwa na Bwana Mwanzo 4 : 10 – 14
- Rahel akamwonea ndugu yake wivu, akafia njiani. Mwz 35 : 16 – 19 na akazikwa tu njiani mahala pasipo rasmi!!
- Sauli akamwonea wivu Daudi akaishia kujiua. 1Samwel 31: 3 – 6
- Absalomu akamwone wivu baba yake Daudi na kutaka yeye ndiye atawale; akaishia kuadhibiwa hata na miti kabla hajauawa!!
2 Samwel 18 : 6 – 15.
- Waliomwonea Yesu wivu waliishia kuliwa fedha zao na ukweli ukaendelea kuhubiriwa. Mt: 28: 11 – 15
Baraka tele juu ya kila mmoja wenu.
–Askofu Dr. L. Mwizarubi
20/4/2014