Social Icons

Sunday, 6 July 2014

HOJA: ONGEZEKO LA IMANI ZA UCHAWI MAKANISANI TANZANIA (6


Msomaji, tulipitia uchambuzi kuhusu “Chanzo Ongezeko la kuogopa uchawi kanisani dalili za kupoteza mamlaka ya Kristo”; tukajifunza “Tafsiri ya misamiati ya “kutoa” na “kupunga” pepo”; Kisha tuligusia juu ya “Huduma za “kutoa pepo” kwa “mtindo” wa “kupunga pepo” na tukajifunza kuhusu “Dalili za “kupunga pepo” badala ya “kutoa pepo” na changamoto zake”. Leo tunaingia sehemu nyingine nyeti kuhusu changamoto za kutumia mitindo ya waganga wa tunguri katika maombezi:
Changamoto ya kutumia mitindo ya
wanganga wa tunguri katika maombezi

Katika uchambuzi wetu kuhusu mitindo ya “kupunga pepo” badala ya “kutoa pepo” katika huduma za maombezi; hatuba budi kuchunguza kimaandiko na kiuzoefu sababu zinazochangia kuwepo kwa mkanganyiko huu na kudhoofisha utendaji wa Roho Mtakatifu katika maombezi ya kufunguliwa.

Huko mwanzo nilionesha hatari ya kuwasiliana na pepo na kupokea na kufanyia kazi ushauri wa
Askofu Sylvester Gamanywa.
kipepo katika kuwaombea watu wafunguliwe na badala yake au matokeo yake watu hawafunguliwi kabisa.

Kwa uchunguzi wangu wa maandiko na uzoefu nilio nao katika huduma za maombezi, nimebaini chanzo kikubwa kimojawapo cha udhaifu ni “matumizi ya misamiati ya waganga wa tunguri” katika huduma za maombezi.
Mfano hai wa jaribio la kuazima misamiati
ya “uganga wa tunguri” katika maombezi
Tangu kushamiri kwa mitindo ya baadhi ya “wachawi wanaotangaza kutubu” na kuachana na uchawi; ambao ghafla watu hao hao kujikita katika huduma za maombezi pasipo kupitia kwanza mchakato wa mafunzo ya Biblia; hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa “matumizi ya misamiati ya kiganga” katika huduma za maombezi.

Tatizo hili lilitaka kujipenyeza katika kanisa la kwanza lakini mitume walilishtukia wakalidhibiti mapema. Tunapata ushahidi wa kimaandiko kutokana na kisa cha mchawi maarufu aliyeitwa Simoni alipotangaza kutubu na kubatizwa katika mikutano ya Filipo. Kilipofika kipindi cha kuombewa ujazo wa Roho Mtakatifu ambacho kiliongozwa na mitume Petro na Yohana, Yule Simoni aliyekuwa mchawi alijikuta anatamani kununua kipawa cha kuwekea mikono watu ili wajazwe Roho Mtakatifu:

“Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemwekea mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu….” (Mdo.8:18-19)
Hapa tunashuhudia mambo mawili kwa Simoni. Kwanza ni tamaa ya kufanya huduma za kiroho kama mbadala wa shughuli za uchawi aliokuwa akifanya hapo awali. Kuwa mkristo kulimwondolea umaarufu wa kufuatwa na watu na kusikilizwa. Akaona njia ya kuendelea na umaarufu wake wa zamani ni kujikitika katika huduma za maombezi ya kikanisa. 
Pili, ni tamaa ya fedha. Alidhani kwamba angeweza kuupata uwezo wa kuwoambea watu ujazo wa Roho Mtakatifu kwa kutoa fedha. Hapa ajenda kubwa na kuombea wengine kwa malipo ya fedha pia, maana hayo ndiyo maisha ya kiganga. Huyu ndiye “Mchawi aliyetubu na kubatizwa” yumo kanisani, lakini kumbe bado kimtazamo binafsi, alikuwa hajafunguliwa katika “kifungo cha uovu” yaani mawazo ya kujipatia umaarufu na mali kwa njia za mazingaombwe! 
Ndiyo maana nilitangulia kutahadharisha kuhusu tabia ya kuwapokea “wachawi wanaotubu” makanisani na kuanza kuwapa madhabahu kushuhudia; na ghafla “kuwageuza kuwa wainjilisti” wakati bado hawajageuzwa kimtazamo wafanyike wanafunzi wa Yesu kweli kweli.
Ndiyo maana watu wa jinsi hii kwa kuwa wanaingia katika huduma za maombezi mapema na bila mafunzo maalum, hujikuta wakirejea katika matumizi ya misamiati ya kiganga (kwa kuwa ndio uzoefu walionao); na kujikuta wakipagawa na tamaa ya kupata mali katika huduma za maombezi badala ya kuwaongoza watu katika kumjua Kristo kikamilifu!
Jinsi Mitume walivyodhibiti
misamiati ya kipepo katika huduma
Tatizo la Simoni kutaka kujikita kwenye huduma za maombezi kwa mitindo ya kiganga lilidhibitiwa na Petro kwa karipio na kemeo kali sana. Makaripio na makemeo ya kitume yameadimika sana makanisani siku hizi. Petro hakumruhusu Simoni alinajisi kanisa kwa mtindo wa kiganga. Soma majibu ya Petro kwa Simoni:

“Lakini Petro akamwambia, fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.” (Mdo.8:20-24)

Ndani ya maandiko haya, ambayo yalikuwa na karipio na kemeo kali la Petro tunajifunza mambo muhimu yafuatayo:
  1. Petro alimwonyesha Simoni kuhusu mtazamo potofu kuhusu matumizi ya karama za Mungu

    Ukisoma kauli za Petro kwa jinsi ya kibinadamu utaona kana kwamba, alimvunjia heshima kwa maneno makali tena hadharani. Bila shaka wachungaji wa siku hizi wangemwita pembeni na kumwonya kwa siri. Lakini, ukweli wa mambo, hapakuwepo na njia zaidi ya kuishughulikia ile roho ya Simoni pale pale pasipo kusubiri.

    Ilibidi ajibiwe waziwazi kwa maneno kama “…kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali…” Hapa Petro alikuwa akiweka msingi wa namna ya kushughulika na upotofu unapojitokeza hadharani kwamba lazima udhibitiwe hadharani na si vinginevyo.
  1. Petro alimwelimisha Simoni kwamba hana sehemu wala fungu katika huduma za maombezi


Kitendo cha Simoni kudai naye anunue uwezo wa kuwapa watu Roho Mtakatifu kinaonesha kwamba tayari Simoni alikwisha kujihesabua haki ya kufanya huduma za maombezi pasipo hata kuidhinishwa na mamlaka ya kikanisa.

Tayari alikwisha kujihesabu kuwa naye ni mmoja wa watoa huduma kwa hiyo alichokuwa anaomba ni uwezo wa kujazwa Roho Mtakatifu na wala si kibali cha kufanya huduma za maombezi. Ndiyo maana Petro ilibidi amwambie waziwazi kwamba “…Huna fungu wala sehemu katika jambo hili…
  1. Petro alimwumbua Simoni hadharani kwamba, bado hajatubia uovu wake;
Kana kwamba hii haikutosha, bado Petro alilazimika kuuweka waziwazi undani wa moyo wa Simoni. Alimwona kwamba moyo wake haujapata badiliko la kitabia tangu alipodai kutubu na kubatizwa. Akamwambia tena: “Tubia uovu wako huu…
Kwa jinsi Petro alivyomkaripia na kumkemea Simoni, ndiyo maana mwitikio wa Simoni haukuwa na ubishi isipokuwa kukiri na kukubali na hata kuomba maombezi ili laana alizotamkiwa zisimpate hata moja. “…Simoni akajibu, akasema, niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja…
Umefikia wakati muafaka kwa kanisa la Tanzania kushika nafasi yake ya kukaripia na kukemea mitindo ya uganga wa tunguri katika huduma za maombezi ili akina Simoni wachawi wanaodai kuwa wametubu; wakajingiza kwenye huduma za maombezi na kuendeleza “misamiati ya kiganga”, wajitathmini upya na kuutubia uovu wao; kwa usalama wa kanisa la roho zao mbele za Mungu.

Itaendelea jumatatu ijayo

No comments:

Post a Comment