Baada ya kusubiri kwa muda mrefu video ya toleo la 'Nisamehe' hatimaye
kwaya kongwe ya Tumaini Shangilieni kutoka kanisa la Mtakatifu James
lililopo Kaloleni jijini Arusha, imekamilisha video hiyo na inatarajiwa
kuwekwa wakfu rasmi jumapili hii, katika ibada zitakazofanyika katika
kanisa lao.
Video hiyo iliyotakiwa kutoka mapema mwaka huu lakini ilishindikana
kutokana na kwaya hiyo kutaka kuifanyia marekebisho ili kukutana na kile
ambacho watu wanakitarajia kupitia uinjilisti wa kwaya hiyo. Mpaka sasa
Tumaini ina matoleo manne ya video na toleo jipya litakalozinduliwa
jumapili linaongeza idadi ya kuwa na jumla ya matoleo matano. Kazi kwenu
mtakao kuwa jijini Arusha jumapili hii, msisahau kufika Kaloleni St
James.
Wakati huohuo baada ya kimya cha muda mrefu cha takribani miaka 10 toka
watoe toleo lao linalofanya vizuri mpaka leo liitwalo 'Tunaishi', kwaya
ya uinjilisti Forest ya kanisa la Kilutheri Forest jijini Mbeya
inatarajiwa kuzindua album tatu mpya za sauti kwa mpigo jumapili hii
katika usharika wao wa Forest wakisindikizwa na kwaya ya Uinjilisti
Kijitonyama ya jijini Dar es salaam pamoja na vikundi vingine vya jijini
Mbeya.
Kwaya hiyo ilikuwa kimya kwa muda mrefu zamani ilikuwa ikijulikana kama
kwaya ya Vijana nasasa Uinjilisti, kati ya nyimbo zao zilizosikika vyema
kutoka katika album iliyopita ya 'Tunaishi', wimbo uitwao 'Wewe Mungu'
ulitokea kuonyeshwa kila asubuhi katika runinga ya EATV na watu wengi
kubarikiwa na ujumbe uliopo kwenye wimbo huo na nyimbo nyingine
zilizokamilisha album hiyo ambayo hata hivyo inapatikana mikononi mwa
kwaya husika baada ya kuiondoa kwa msambazaji wao.
No comments:
Post a Comment