Mungu anasema mengi sana kuhusiana na moyo. Lakini moyo ni nini? Na umuhimu wa moyo ni nini katika maisha yetu ya kiroho na ya kimwili?
Hebu angalia maandiko machache yafuatayo na uone kile ambacho Bwana anasema kuhusiana na moyo.
Naye akanifundisha, akaniambia, moyo wako uyahifadhi maneno yangu; shika amri zangu ukaishi. (Mith 4:4).
Mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. (Mith 3:1).
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. (Zab 119:11).
Yafunge hayo katika moyo wako daima; jivike hayo shingoni mwako. (Mith 6:21).
Maandiko haya yanaonyesha kuwa sheria ya Mungu inatakiwa kushikwa au kuwekwa kwenye moyo. Je, maana yake ni nini? Pia inaashiria kuwa huwa hatuweki sheria yake mioyoni mwetu. Je, huwa tunaiweka wapi badala yake?
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe (Mith 3:5).
Ninatakiwa kumtumaini Bwana kwa moyo; sio kwa akili. Hii maana yake ni nini? Kuna tofauti gani kati ya moyo na akili hapa?
Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako (Kumb 6:6).
Mungu anaposema kuwa maneno yake yawe kwenye moyo wangu, anaamanisha yasiwe wapi?
Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. (Mith 4:23).
Hii inaonyesha kuwa moyo ni wa muhimu sana. Kumbe uzima unatokea moyoni! Lakini je, moyo unalindwaje?
Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini? (Yer 4:14).
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. (Mt 5:8).
Je, moyo unaoshwaje? Kuna uhusiano gani kati ya uchafu wa moyo na mawazo?
Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo. (Efe 3:17).
Kristo anakaaje moyoni kwa imani? Nitajuaje kuwa Kristo sasa yuko moyoni mwangu? Nifanye nini ili Kristo akae moyoni mwangu?
Rafiki mpendwa, mambo ya Mungu wetu ni rahisi mno! Tatizo letu ni ukosefu wa maarifa tu! Bwana anasema:
Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya. (Kumbukumbu 30:11-14).
Mpendwa, iko siri ya ajabu sana kuhusiana na mioyo yetu. Humo ndimo kuna kila kitu tunachohitaji ili kuwa washindi katika maisha haya na yale yajayo.
Fuatana nami katika sehemu ya 2 ya somo hili muhimu sana. Mwisho wa yote utafurahia hakika kile ambacho Bwana ametuandalia. Tena utaelewa nini maana ya andiko hili:
Yote yawezekana kwake aaminiye. (Marko 9:23).
Mwanadamu alivyoumbwa
Tukisoma Biblia kuhusiana na uumbaji wa mwanadamu, imeandikwa hivi:
Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. (Mwanzo 2:7).
Kulingana na andiko hili, tunajifunza yafuatayo:
(a) Mwanadamu ana sehemu kuu mbili.
(b) Sehemu ya kwanza ni mavumbi, yaani mwili unaoonekana
kwa nje na tunaweza kuugusa.
(c) Sehemu ya pili ni pumzi ya uhai ambayo iko ndani na hatuwezi
kuiona wala kuigusa.
(d) Mavumbi pamoja na pumzi ya uhai yanaunda nafsi hai.
Tunafamu kuwa mwanadamu aliye hai ana hisia, mawazo, akili, utashi
na kumbukumbu. Lakini haya yote ni mambo yasiyoonekana kwa macho ya
nyama – ila tuna uhakika kabisa kuwa yapo.
Vilevile, tunafahamu kuwa mtu akifa, mwili unaobakia hauna hata moja kati ya mambo hayo hapo juu, yaani:
- Hauwezi kuhisi
- Hauwezi kuwaza
- Hauna akili
- Hauna utashi
- Hauna kumbukumbu.
Hili linatupa ishara kuwa, mambo haya ni sehemu ya ile pumzi ya
uhai. Tunasema hivi kwa sababu, tunaposoma habari ya tajiri na Lazaro
kwenye Luka 16:19-31, tunaona kwamba:
(a) Ana hisia ndiyo maana anateseka kwa joto
(b) Ana mawazo na akili, kumbukumbu na utashi ndiyo maana
anawafikiria ndugu zake waliokuwa duniani na anaamua
kuomba msaada kwa Ibrahimu ili yamkini Lazaro aende
kuwapelekea maonyo kule duniani.
Lakini, ni wazi kuwa mambo hayo yote, mwili wake uliobakia duniani
hauna kamwe uwezo wa kuyafanya.Kumbe basi, pumzi ya uhai ndiyo inayobeba
mambo haya yote ambayo hayaonekani wala kugusika. Haya ni sehemu ya
yule mtu wa ndani, ambaye adumu milele.
Pumzi ya uhai
Tukiachana na mwili sasa, hebu tuangalie huyu mtu wa ndani kwa ukaribu zaidi.
Biblia inasema kuwa: Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu
(Yohana 6:63). Pia inasema: Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa …
(Yakobo 2:26).
Kumbe basi, mtu halisi ni roho. Roho ni mtu mwenye umbile kama
ulivyo mwili wetu wa nyama (mavumbi). Na roho ikitoka inaondoka na yale
yote yasiyooneka huku mwili ukibakia bila ufahamu hata chembe.
Hii roho ndiyo yule mtu wa ndani kwa ujumla wake; ndiyo ile pumzi
ya uhai aliyopulizia Mungu ndani ya mavumbi. Na ndani ya hii roho ndimo
ulimo moyo na akili na utashi, n.k.
Kielelezo kifuatacho kinaweza kutusaidia kuelewa kirahisi haya
ambayo tumeyasema hadi hapa. Sina uhakika kabisa iwapo moyo unakaa
kichwani tu na kwenye mwili wote kama roho. Ila hiki ni kielelezo tu
kuonyesha uhusiano ulivyo. Huenda moyo umejaa kila sehemu. Ila
ninachojua tu ni kwamba, upo.
Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu,
kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini,
na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia,
na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
(Mwanzo 1:26).
Tazama nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge,
na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu
kitakachowadhuru. (Luka 10:19).
‘Kutawala’ ni kuwa na mamlaka, amri au usemi wa mwisho juu ya jambo
au hali. Hii ina maana kwamba chochote kilicho chini ya mamlaka hayo
hakiwezi kufanya kilicho juu ya mamlaka hayo iwapo mamlaka yenyewe
yamesimama sawasawa.
Biblia inasema: Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).
Lakini swali la msingi ni kwamba, je, hatujasikia? Je,
wanaoumwa ni wale ambao hawajawahi kusikia Neno lisemalo: Kwa kupigwa
kwake sisi tumepona (Isaya 53:5)? Je, wenye hofu ni wale tu ambao
hawajasikia kwamba Bwana ameshasema: Maana Mungu hakutupa roho ya woga,
bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi (2 Timotheo 1:7)?
Jibu ni HAPANA! Tayari tumeshasikia na kusikia na kusikia ….!
Inakuwaje basi lisitimie kwetu neno lisemalo: Basi imani, chanzo
chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo; ili kwamba imani
hiyo ituwezeshe kushinda katika kila jambo? Mbona tunazidi kulemewa na
shida za dunia hadi tunakata tamaa na hata kufikia kumwacha Kristo? Au
huku kusikia kunakotajwa kwenye Warumi 10:17 ni tofauti na maana
tunayoijua ya neno hilo?
Imeandikwa kwamba: Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. (Mathayo 15:18).
Na tena: … Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu
mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya
hutoa mabaya. (Mathayo 12:34-35)
Kwa kuwa: Yote yawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23), basi, kushindwa kwangu kuna maana kwamba sina imani; pia sijasikiakwa jinsi ambayo itaniwezesha kupata hiyo imani inayoweza yote!
Na kwa kuwa Bwana anasema katika Waefeso 3:20 Basi atukuzwe yeye
awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo,
kwa kadiri ya nguvu itendayo kazindani yetu, (na si kwa kadiri ya nguvu itokayo juu mbinguni), ina maana kwamba tatizo limo ndani yangu, yaani kwenye moyo.
Ukiniuliza kuhusu maandiko mbalimbali na ahadi za Mungu, ninaweza
kukutajia moja baada ya jingine. Lakini iwapo sina nguvu ya kugeuza hali
yangu, ina maana kuwa ninajua tu kwa akili lakini si kwa moyo. Ni nguvu
itokayo moyoni tu ndiyo inayobadili mambo! Kwa hiyo, kama Neno la
Kristo halimo moyoni mwangu, basi humo kuna neno la mwingine!
Kwa nini nimejawa na hofu, mashaka, wasiwasi, huzuni, kukata tamaa,
n.k. ilhali hakuna kokote kwenye Biblia ninakoagizwa kuwa hivyo? Ni kwa
sababu hayo ndiyo yaujazayo moyo wangu – ndiyo maana yananitoka muda
wote.
Kumbe basi imani ninayo; isipokuwa tu nina imani na neno la adui.
Nimesikia neno la adui – na hilo ndilo ambalo limeujaza moyo wangu.
Neno la adui linasemaje? Linasema:
Huwezi!
Hufai!
Umeshindwa!
Hauna nguvu!
Haufiki popote!
Una dhambi!
Wewe ni maskini!
Hautapona!
Maisha ni magumu!
Hawakupendi!
Hujasoma!
Utashindwa tu!
Unapoteza tu muda!
Kazi hazipatikani kirahisi!
Bila kutoa kitu kidogo hutafanikiwa!
Wengi walishajaribu wakashindwa!
n.k, n.k, n.k …..!
Neno hili linatokea wapi? Mungu ana kitabu cha Biblia lakini
shetani hana kitabu kilicho wazi. Lakini anayo ‘injili’ yake mbaya. Neno
lake linakuja kwetu tangu tunapozaliwa. Neno hilo linatokea kwa wazazi,
ndugu, walezi, majirani, marafiki, redio, televisheni, muziki,
magazeti, wanasiasa, wapita njia, n.k.
Tunalisikia neno hili karibu muda wote. Matokeo yake, bila hata
sisi kujua, neno hili limejaa tele mioyoni mwetu na ndilo limekuwa
sehemu ya mawazo yetu na miwani ambayo kwayo tunayaona na kuyapima
maisha.
Je, Mungu ni mwongo? Hapana!
Je, Mungu hajui anachokisema? Hapana!
Je, Mungu ana uhakika kabisa na kile anachosema? Ndiyo!
Kama basi ni kweli amenipa mamlaka au amri juu ya vyote kama
anavyosema kwenye Mwanzo 1:26, je, ina maana kwamba ninayo amri juu ya
nyoka, samba, nge, moto, mafuriko, mvua, ukimwi, utasa, ajali na hata
mauti?
Kwa kuwa Mungu si mwongo, jibu ni NDIYO!!!!
Kama hivi ndivyo, basi tatizo si Mungu; wala tatizo si Neno lake,
bali ni habari ya ndani ya moyo wangu; maana imeandikwa: … atukuzwe yeye
awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au
tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu (Waefeso 3:20).
Kusikia kunakotajwa kwenye Warumi 10:17 si suala tu la sauti ya
muhubiri kupenya ndani ya masikio yangu. Hapana! Ni zaidi ya hapo.
Udongo mgumu ukinyeshewa na mvua kwa mara moja kisha jua likauwakia
kwa siku 7, utaukuta ni mkavu – lakini kuna mvua iliunyeshea! Lakini
ukinyeshewa kwa siku 7 na kuwakiwa na jua kwa siku moja, utaukuta ni
mbichi.
Sisi nasi, kama udongo, tumeshasikia na kusikiliza (kutafakari)
mambo mabaya (neno la adui) tena na tena maishani mwetu kuliko
tulivyofanya kwa Neno la Kristo. Hivyo, mvua ya neno la adui imeweza
kupenya ndani sana kwenye mioyo yetu. Kwa hiyo, ile nguvu itendayo kazi
ndani yetu ni nguvu ya adui, ambayo ni nguvu ya uharibifu na kushindwa.
Imani chanzo chake ni kusikia. Imani ya kushindwa imejaa kwetu na kuwa
na nguvu kutokana na kusikia zaidi neno la adui!
Pamoja na kwamba tumeshasikia karibu kila Neno la Bwana wetu Yesu,
maandiko hayo hayajatufaa sana maana kinachoendelea ni kama kunyeshewa
na mvua ya siku moja ya neno la Bwana na kuwakiwa na jua la siku 7 la
neno la adui.
Hebu tujipime kama tunatenda sawasawa na vile inavyotakiwa. Je, Bwana mwenyewe anasemaje?
- Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana (Yoshua 1: 8).
- Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu; naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu (Mithali 2:1-5).
- Nawapenda wale wanipendao, na wake wanitafutao kwa bidii wataniona (Mithali 8:17).
- Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
- Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye (Kutoka 15:26).
Naamini wengi wetu tutakubaliana kwamba kipengele cha bidiikatika
kusikiliza, kusoma na kutafakari Neno la Kristo kimekosekana kwetu.
Sasa, kama hakipo inawezekana Neno hilo likafika moyoni ambako ndiko
linatakiwa kuzalisha nguvu ya kutushindia?
Mimi ninapotembea njiani, ninapokuwa kwenye daladala, n.k., huwa
nasikia mechi za mpira zikitangazwa. Lakini kwa kuwa mimi si shabiki wa
mpira maneno hayo huwa tu ni kama mvua ya siku moja kwenye udongo mgumu.
Hata timu inapofunga na watu wanaruka na kushangilia kwa kelele nyingi,
kwangu hata kamsisimko kadogo sipati kabisa – lakini ninakuwa nimesikia
mtangazaji akisema, “Gooooo!” Ni masikioni tu, lakini neno lake
halivuki zaidi ya hapo.
Lakini hebu mwangalie shabiki mwenyewe wa mpira. Yuko makini
kusikiliza na kufuatilia kila neno la mtangazaji. Hata ukimsemesha,
anaweza akakasirika kwa hasira ya kweli kabisa! Kwa nini? Hataki apitwe
hata na neno moja. Yuko makini kweli kusikiliza kila kitu. Anasikiliza
kwa bidii.
Kwa umakini huo, ni lazima kile anachosikia kinapenya moja
kwa moja hadi ndani kabisa. Ndiyo maana kinazalisha hata nguvu ya kuruka
na kupiga kelele pale timu yake inapofunga; au nguvu ya kulia na
kushindwa kula timu hiyo inapofungwa. Kwa nini? Ni kwa sababu kile
anachokisiliza anakipa nafasi yote ya kufika hadi ndani kabisa kwenye
mtambo wa kuzalishia nguvu – yaani moyo.
Neno la Kristo lina nguvu kubwa sana ya kutenda chochote
alichoahidi Bwana pale tu tutakapolipa nafasi ya kufika kwenye moyo – si
kwenye ubongo (akili)!
Je, shabiki wa mpira hufanya mazoezi ya kushangilia au kulia kabla
ya kuanza kusikiliza mechi? Hapana! Anachofanya ni kutoa tu umakini;
kusikiliza kwa bidii kile kinachotangazwa. Kisha lile neno la mtangazaji
lenyewe linazalisha nguvu ama ya kukasirika, kushangilia au kulia.
Imani chanzo chake ni kusikia neno kwa bidii zote. Yaani, kile
tunachosikia, kikifika tu moyoni, kinageuka na kuwa imani
‘automatically’. Kwa hiyo, kama bidii yetu tumeiweka kwenye kusikia
zaidi neno la adui, itazaliwa imani ya kushindwa. Kama bidii yetu ni
katika Neno la Kristo, itazaliwa imani ya kushinda.
Mpendwa, usifanye bidii kutafuta imani. Fanya bidii kutafuta Neno.
Hata Biblia nayo inasema: Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee
imani (Luka 17:5).
Lakini Bwana alifanya nini? Badala ya kuwaongezea, aliwaambia:Kama
mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu,
Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii (Luka 17:6).
Imani haiongezwi kutoka kwa Bwana. Imani inatokea ndani pale Neno
linapopewa nafasi kufika hadi moyoni. Bidii kubwa kwetu iwe ni katika
kuingiza Neno la Bwana wetu kwenye mioyo yetu. Imeandikwa: Neno la
Kristo na likae kwa wingi ndani yenu(Wakolosai 3:16).
Hatuwezi kupiga hatua yoyote ya maana kama muda mwingi tunasikiliza ya dunia – ambayo kwa sehemu kubwa ni ya adui.
- Hebu tujipime kidogo kwa maswali machache yafuatayo:
- Je, una ugonjwa wa muda mrefu? Je, unawaza zaidi mawazo ya Kristo ya kupona au ya adui ya kutopona?
- Je, haujaolewa? Je, unawaza zaidi kuwa utaolewa au unawaza zaidi kuwa umri unakwenda?
- Je, hauna kazi?
- Je, haujapata mtoto?
- Je, kuna dhambi inayokutesa?
- Je, unakabwa na wachawi kila siku?
- Je, biashara yako haiendi vizuri?
- Je, unafeli masomo darasani?
- Je, una shida gani maishani mwako?
Swali kuu sasa ni je, unawaza zaidi Neno la Kristo juu ya hali yako
au neno la adui? Ni kweli unaweza pia kuwa na maandiko yenye ahadi za
Mungu kuhusu hali yako, lakini je, yako moyoni au yako kichwani tu? Cha
moyoni ndicho cha maana. Sasa hicho ni Neno la Kristo au ni neno la
adui?
Neno la Kristo likifika moyoni utajua tu, maana hofu na mashaka
yote yataondoka kwako. Lakini kama hofu na mashaka bado vimo ndani yako,
basi ni wazi kuwa neno la adui ndilo lililoko moyoni; na imani iliyomo
ni ya kushindwa.
Tunafikishaje Neno la Kristo moyoni?
- Kusoma Neno la Kristo (Biblia) zaidi na zaidi na zaidi. (Kumbuka, tunazo hofu na mashaka kwa kuwa tunasikia neno la adui zaidi na zaidi na zaidi).
Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku,
upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo;
maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi
sana (Yoshua 1: 8).
- Kutafakari Neno la Kristo na mambo mema zaidi na zaidi na zaidi.
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote
yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote
yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo
sifa nzuri yo yote,yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
Tukijichunguza wenyewe, tutagundua kuwa muda mwingi huwa tunawaza kushindwa, kukosa, kukosea, kupoteza, kufa, n.k.- Kunena kwa lugha zaidi na zaidi na zaidi.
Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake (1Wakor 14:4).
- Kufunga na kuomba ili kutiisha mwili. Kumbuka kwamba hatufungi ili kumshawishi Mungu atufanyie mambo tuyatakayo. Mungu alishafanya kila kitu tayari kwa ajili yetu (Waefeso 1:3).
Tunafunga ili kwamba mioyo yetu iweze kuwa katika mstari sahihi unaoruhusu kupokea kile amacho tayari tulishapewa na Baba yetu.
Mwanafunzi anapoacha kitanda chake na kwenda kusoma usiku, hafanyi
hivyo ili kumshawishi mwalimu ampe maksi nyingi. Bali anafanya hivyo ili
kuiweka akili kwenye mstari unaoruhusu yeye kupokea maksi nyingi
kulingana na yote ambayo mwalimu tayarianakuwa amemfundisha.
Kukataa kwa makusudi kila jambo la kidunia ambalo ni kinyume na
Neno la Kristo – iwe ni muziki, sinema, matangazo ya biashara,
mazungumzo mabaya, n.k.
Kwa mfano, muziki wa kidunia unavutia sana. Lakini huo ni ujumbe wa
mauti. Hauna uzima ndani yake. Na kati ya vitu vyenye nguvu na uwezo
mkubwa wa kwenda moja kwa moja hadi moyoni ni muziki. Labda mtu
atasingizia kwamba anajiburudisha na kujipatia mafunzo mbalimbali kutoka
humo. Huo ni uongo wa kuzimu na udanyanyifu wa moyo (Yer 17:9).
Shida ya imani, kama tulivyoona, ni kuwa, inazalishwa na neno
linaloingia moyoni – si kwa juhudi za mwanadamu. Pasipo kujua, utajikuta
unayo tu hiyo imani. Kumbe imetokana na neno la adui lililoingia moyoni
kupitia bongofleva, sinema, magazeti ya udaku, n.k.
Hitimisho
Moyo ndiyo sehemu ya muhimu kuliko zote kwa mwanadamu. Ndiyo maana hata Bwana akasema: Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima(Mithali 4:23).
Bidii yetu ni katika kulifikisha Neno la Kristo mioyoni. Kisha Neno hilo litafanya mengine YOTE yanayosalia. Bwana anaahidi:
Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;
ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.
Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima
na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.
Badala ya michongoma utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia Bwana jina, Litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali (Isaya 55:10-13).
Ardhi haifanyi chochote zaidi ya kunywa tu maji ya mvua. Kisha mvua yenyewe (sio ardhi), inachipusha mimea kwenye ardhi.
Neno la Kristo likiingia kwenye moyo kwa wingi, ahadi zote za Bwana
zitachipuka tu!! Lazima!! Hata kama ibilisi na mashetani wote
wangepinga kiasi gani, lazima Neno la Kristo litashinda tu!! (maana
tusisahau kuwa upinzani ni lazima uko palepale).
Tahadhari
Katika makala yangu mengine niligusia kwamba moyo ndiyo kile
ambacho wanasaikolojia huita ‘sub-conscious mind’. Ukisoma kwenye
mtandao au kwingineko, utakutana na masomo yanayosema: “How to use the
power of the sub-conscious mind to obtain anything you want in life”,
yaani “Kutumia nguvu ya akilifiche kupata chochote ukitakacho maishani
mwako.”
Masomo ya namna hii ni hatari sana kwa sababu kimsingi hii ni ibada
ya sanamu (idolatry). Ibada ya sanamu ni kutumainia kitu kingine
chochote (au wewe mwenyewe) badala ya Mungu wa Ibrahimu, Isaka na
Yakobo.
Nguvu yetu inatoka kwa Bwana pekee. Anasema wazi: Mtumaini BWANA
kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe (Mithali 3:5).
Na tena anasema: … pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno
lolote. (Yohana 15:5).
Watu wanaofundisha masomo haya wanasema, kimsingi, kuwa
sub-conscious mind ina uwezo wa kufanya lolote litokee kama unavyotaka,
maadamu tu uwe na shauku kubwa ya kuyapata na kuamini kabisa kwamba
itayatenda hayo.
Huo ni mtego wa adui utakaosababisha tujitenge mbali na Mungu wetu na kujitumainia wenyewe.
Hebu basi na tufanye bidii katika kuondoa usikivu wetu kwa dunia
ili Neno la Kristo liweze kukaa kwa wingi muda wote mioyoni mwetu.
Hakika Neno hilo litaichipuza ardhi ya mioyo yetu kulingana na yale
yaliyo shauku za mioyo yetu.
Na imani inakua kadiri tunavyozidisha bidii ya kusikia!
Sasa, kama ni neno lenyewe ndilo linaloumba imani; ndilo
linalotenda kile alichoahidi Baba yetu wa Mbinguni – ilhali kazi yetu ni
kuliingiza tu ndani yetu kupitia bidii ya kusoma, kutafakari,
kusikiliza, n.k., je, unaona sasa maana ya maneno ya Bwana wetu kwamba:
YOTE YAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE (Mk 9:23)?
Sisemi kuwa ni rahisi, bali ninasema kuwa INAWEZEKANA maana Bwana
ndiye anayetenda kazi ndani yetu! Kwa kuwa: Mungu akiwapo upande wetu,
ni nani aliye juu yetu? (Warumi 8:31).
Bwana Yesu akubariki na kukutia nguvu mpendwa msomaji na ndugu yangu.
–Injili ya Kweli blog
NA
No comments:
Post a Comment